Ushuhuda (I.N.)

 
Ilikuwa usiku wa tarehe 28 Disemba 2021, tukiwa katika zoezi la kutahajudi, mwalimu wetu aliyekuwa akituongoza alikuja na kunigusa. Niliona mwanga Mweupe, ambao baadaye ulififia na kisha likaja ua hili kubwa la zambarau lililochanua.

Kesho yake tuliendelea na tafakari, siku hii nilianza kusikia sauti za vitu, baadaye nikawa nasikia sauti kama mawimbi ya maji ya mto unaotiririka, na sauti nyembamba sana za ndege kwa mbali, nilipenda sana kuendelea kuzisikiliza hizo sauti kwani ilionekana ni eneo lenye amani na utulivu.

Safari haikuishia hapo bado tuliendelea na zoezi, katika majira ya jioni, nikiwa katika zoezi la mwanga na sauti, nikiwa katika hali ya utulivu kupitia paji la uso, niliona tena mwanga mweupe sana, mbele yangu, nilivutiwa na nilitamani kuufikia, nilianza safari ya kuuendea ule mwanga, kwa kuwa ulikuwa mkali mithiri ya mwanga wa jua.

Nilihisi kama hofu iliyotaka niache kuusogelea na kuutazama ule mwanga na nirudi nyuma, ila kabla ya kufanya maamuzi hayo ya kurudi nyuma, nilisikia sauti ndani yangu ikiniambia “usiongope hiyo ni akili inakutaka urudi nyuma”, nilipogeuka nikaona kama kivuli, nikapata ujumbe kuwa ile ndio Hofu, kisha niliendelea mbele kuelekea pale ambapo mwanga ulikuwepo.

Nilifanikiwa kuufikia hatimaye nikauvaa ule mwanga nao ukanivaa, tukawa kitu kimoja, Mimi nikawa mwanga na mwanga ukawa ndio Mimi.

Majira mengine tena tuliendelea na tahajudi, ni kama vile niliendelea nilipokuwa nimeishia, nilisafiri Mimi Kama mwanga, kisha nikasikia kama sauti ya kike kwa mbali, ikisema hello haukupita muda mrefu nikasikia tena sauti ya kiume hii ilikuwa karibu lakini sikumuona mtu yeyote isipokuwa nilipata ufahamu juu ya uwepo wa mtu.

kisha akaanza kuniambia ile sauti ya kike uliyoisikia ndio Mimi hakuna mwanamke wala mwanaume, nimekuja ili kukuongoza ule mwanga na ile sauti uliyekuwa unaitafuta ndio mimi, wakati huo sikuweza tena kuisikia ile sauti ikitoka nje yangu, bali ilikuwa ikitokea ndani yangu.

Ile sauti iliendelea kwa kuniambia sasa si unataka nikupeleke hadi mahali ambapo Mungu yupo, nikasema ndio, kisha akachora Kama S iliyotokea kama bahari, yenye mwanzo na mwisho, akaniambia hii haikuwepo ila sahizi imetokea, sasa nitakuongoza huko unakotaka kwenda kwa Mungu, ila ujue kabisa, mimi Kama mwanga na sauti sitafika yaani kuna mahali sitakuwa nawe kwa kuwa mahali hapo hakuna kitu chochote.

Siku ile nayo ilipita, siku iliyofata wakati wa meditation mimi nikiwa kama mwanga unaong’a sana nilisafiri kwa kasi sana, katika mwendo huo nilikuwa nikiimba nikisema nimeumaliza mwendo, sikuweza kuona chochote, kadiri nilivyozidi kusafiri ndivyo ile sauti na umbo langu vilivyozidi kupungua, sauti ikapotea na umbo nalo likazidi kupungua lilipungua hadi ikabaki kama nukta, ambapo nayo baadaye ilipotea.

Sikuweza kujua na kutambua chochote kwa muda fulani, isipokuwa baada ya muda fulani tena nikawa najiona ni kama nukta ndogo sana ambayo ilianza kukuwa na hatimaye Kuwa kama umbo la mtu lililokuwa liking’aa sana.

Kutokea hapo nikaianza tena safari ya kurudi, wakati huu navyorudi nilikuwa nashuhudia uumbaji wa mimea yenye majani laini, pia niliona uwepo wa miale mizuri sana ya kama jua linaloanza kuchomoza asubuhi, hakika nilishuhudia mandhari ya asili yenye kupendeza na kuvutia sana.

Ndipo nikakumbuka kuwa ule wakati nilipochorewa ile bahari, ni kuwa nitashuhidia uumbaji wakati huohuo.

Haya yalitokea wakati wa uanzishwaji wa safari ya mwanga na sauti.

Baadaye tulirejea nyumbani, hapo nikiwa kama mtu mpya, ambapo hali ya utulivu, amani, upendo, furaha vikiwa vimekuwa kwa kiwango cha juu zaidi, pia hali na kiu ya kutahajudi ilikuwa zaidi, nilianza kujua matukio ya kimaisha yaliyo mbele yangu, kupata majibu, ya maswali yangu ya kiroho na kimwili.

Kuna Siku nyingine nikiwa nyumbani wakati wa meditation nilisafiri tena hadi kufika katika eneo lile ambalo hamna kitu, nami nikawa Hanna kitu. Ila safari hii ilikuwa tofauti na ile ya kwanza, kwani awamu hii nilishuhudia vitu vingi sana njiani, ikiwepo sayari iliyojawa na madini tu yaliyokuwa yakielea(sayari ya dhahabu), niliwaona viumbe wengi wanaojulika kama aliens wakiwa katika mji wao.

Pia navyorudi nilishudia uumbaji wa vitu vya asili kama ule wa mwanzo, wakati nashuhudia vitu vikitokea, ghafla nikaona nimekuwa mwanga mkali sana zaidi hata huu wa jua tunao uona huku duniani, katika hali hiyo nikiwa kama jua lililo kwenye chanzo, nikiwa huo mwanga nilijiona nanamulika kila mahali na kila kona, nilipata ujumbe kuwa sasa naona na kufahamu kila kitu, japo sikuona kitu chochote zaidi ya huo mwanga.

Katika safari, Nimebaini kuwa mimi ndio muumbaji, mimi ni upendo, mimi ni Alfa na omega, mimi ni kila kitu, na kila kitu ni mimi.

Nashukuru sana walimu, kila mtu na kila kitu, ulimwengu na nisharti ya mwanga na sauti kama nguvu ya uhai, iliyo kwenye kila kitu na inayounganisha kila kitu na kila kitu.

Nionapo chochote najiona Mimi, na hakuna umbali kati yangu na chochote kile kwani Mimi ndio kila kitu na kila kitu ndio Mimi.

LIFE IS ENERGY AND LOVE IS LIFE.
LOVE YOU MORE.